Wakati uhusiano wa kibiashara kati ya Kenya na China ukiendelea kupanuka, Kenya Jumatatu iliandaa mkutano wa kiuchumi na kibiashara mjini Nairobi na kushirikisha wajumbe wa ngazi ya juu kutoka mji wa Shenzhen nchini China.
Mkutano huo pia ulivutia wawakilishi wa karibu makampuni 100 ya biashara wa ndani na wawakilishi wa China wanaoishi ng'ambo kutoka Chama cha Wafanyabiashara cha Kenya.
Rais wa Chama cha Kitaifa cha Wafanyabiashara na Viwanda cha Kenya, Eric Ruto, alisema makampuni ya ndani yana shauku ya kushirikiana na viwanda vya utengenezaji bidhaa vya Shenzhen kutokana na teknolojia yao ya hali ya juu katika sekta zinazopewa kipaumbele nchini Kenya, hasa katika nyanja za matibabu, elektroniki na nishati mbadala.
Naye mkuu wa Wilaya ya Bao'an huko Shenzhen, Wang Lide, alisema wilaya yake imetengeneza faida linganishi katika bidhaa za matumizi za kielektroniki, vifaa vya nishati mpya, bidhaa za optoelectronic, vifaa vya elektroniki, vifaa vya umeme vya semiconductor, mashine za kuchomelea za ultrasonic, na vifaa vya matibabu.