Wizara ya Afya nchini Kenya imeridhia matumizi ya vipimo vitatu vya UKIMWI vilivyopendekezwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) kwa ajili ya utambuzi sahihi.
Katibu wa kudumu wa Wizara hiyo Harry Kimtai amesema katika taarifa yake iliyotolewa jana jijini Nairobi kuwa, njia hiyo mpya inahakikisha uaminifu na usalama wa huduma za vipimo. Amesema wafanyakazi wa afya na jamii wanatakiwa kuunga mkono juhudi zinazoendelea za kudumisha uaminifu wa huduma za upimaji, na wananchi pia wanatakiwa kutumia huduma mpya za vipimo kote nchini humo.
Kwa mujibu wa WHO, mkakati wa vipimo vitatu unatumia vipimo vya UKIMWI ili kutoa utambuzi wa uhakika, na hivyo kuhakikisha kuwa upimaji wa UKIMWI unawafikia wengi na kudumisha kanuni ya mtu binafsi kuridhia, usiri, ushauri, matokeo sahihi na huduma zinazohusika.