Majaribio ya Kuifanya Taiwan Ijitenge na China kamwe hayatafanikiwa
2024-05-29 10:50:23| cri

Mkutano wa 77 wa Baraza la Afya Duniani (WHA) umekataa kwa mara nyingine tena kile kinachoitwa pendekezo la “kuialika Taiwan kushiriki katika mkutano wa baraza hilo kama mwangalizi”. Huu ni mwaka wa nane mfululizo kwa Baraza hilo kukataa pendekezo kama hilo, ikionyesha kuwa, kanuni ya kuwepo kwa China moja imekuwa maoni ya pamoja ya jumuiya ya kimataifa. Jaribio la Mamlaka za Chama cha Demokrasia na Maendeleo cha Taiwan (DPP) la kutegemea nguvu za nje kufanya mbinu za kisiasa linaharibu maslahi ya dunia na pia kujidhalilisha, na majaribio ya kuifanya “Taiwan ijitenge na China” kamwe hayatafanikiwa. 

Hivi sasa dunia iko katika hatua muhimu ya kuimarisha ushirikiano wa afya. Mkutano huo utajadili masuala makuu kama vile marekebisho ya Kanuni za Kimataifa za Afya, na Mkataba kuhusu Majanga Makubwa (Pandemic PACT). Hata hivyo, mamlaka ya Taiwan na nchi kadhaa zinajaribu kufanya mbinu za kisiasa, na kutanguliza maslahi yake ya kibinafsi ya kisiasa mbele ya usalama wa afya ya umma wa kimataifa, kitendo ambacho lazima kilaumiwe na jumuiya ya kimataifa.

Kuna China moja tu duniani, na Taiwan ni sehemu isiyotengeka ya China. Haijalishi njama zinazofanywa na mamlaka ya DPP na nchi chache, ukweli huu hautabadilika. Kanuni ya Kuwepo kwa China Moja haitabadilika, na majaribio ya kutafuta kuifanya Taiwan ijitenge na China, na kuidhibiti China kwa kutumia suala la Taiwan hakika yatashindwa.