Nchi za Afrika zilizo Kusini mwa Sahara zinapaswa kuchunguza njia bunifu za kutafuta mtaji kutoka benki za ndani, hatifungani za serikali na mifuko ya Hifadhi ya Jamii ili kuharakisha ukuaji unaostahimili tabia nchi.
Hayo yamesemwa Jumatano na watendaji wakuu wakati walipozungumza kando ya mkutano wa mwaka wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) unaofanyika jijini Nairobi, Kenya ukiwa na kaulimbiu ya "Mabadiliko ya Afrika, Kundi la Benki ya Maendeleo ya Afrika, na Marekebisho ya Usanifu wa Fedha Duniani." Watendaji hao walibainisha kuwa ni muhimu kwa nchi hizo kuzingatia soko la ndani ili kukabiliana na upungufu wa ufadhili wa kijani.
Mkuu wa Nishati na Miundombinu katika Afrika Mashariki wa Benki ya Standard, Mphokolo Makara, alisema masoko ya mitaji ya Afrika na sekta binafsi zinaweza kusaidia kuziba pengo la ufadhili linalozuia hatua za mabadiliko ya tabianchi barani humo.
Kwa mujibu wa Rais wa AfDB Akinwumi Adesina, Afrika inapokea dola za Kimarekani bilioni 30 tu katika ufadhili wa tabia nchi kila mwaka, zikiwa ni kidogo sana ikilinganishwa na dola bilioni 277 zinazohitajika, na kufanya kupunguza kasi ya mabadiliko ya kijani barani.