Wataalamu wakutana nchini Kenya kujadili sera za kodi barani Afrika
2024-05-30 08:59:30| CRI

Wataalamu walikutana Nairobi, Kenya, Jumatano kujadili mikakati ya kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani kupitia hatua madhubuti za kodi barani Afrika.

Mkutano huo wa 9 wa Kodi Afrika wa mwaka 2024 ambao unaendelea kwa siku tatu umewaleta pamoja wajumbe zaidi ya 200, wakiwemo wasimamizi wa kodi wa Afrika na washirika wa maendeleo, kushughulikia masuala muhimu ya kodi kama vile mapato kutokana na biashara za kuvuka mipaka.

Kamishna mkuu wa Mamlaka ya Mapato ya Kenya, Humphrey Wattanga Mulongo, alizitaka nchi za Afrika kufanya usimamizi wa kodi na ukusanyaji wa mapato kuwa wa kisasa licha ya kukabiliwa na changamoto kama vile uzembe, ukosefu wa uongozi mzuri na mtiririko haramu wa fedha.

Pia alitoa wito kwa wasimamizi wa kodi wa Afrika kulinda haki za walipa kodi, kuzingatia uadilifu, haki, na uwajibikaji wakati wa kuwahudumia, na kufanya mifumo madhubuti ya utatuzi wa migogoro kufikiwa kwa urahisi.