Rais wa China ahutubia ufunguzi wa mkutano wa 10 wa mawaziri wa Baraza la Ushirikiano kati ya China na Nchi za Kiarabu
2024-05-30 11:05:48| cri

Rais wa China Xi Jinping ametoa hotuba kwenye ufunguzi wa mkutano wa 10 wa mawaziri wa Baraza la Ushirikiano kati ya China na nchi za Kiarabu

Katika hotuba yake, rais Xi amesema, China iko tayari kushirikiana na nchi za kiarabu kwa kusaidiana na kuimarisha uhusiano wao kuwa mfano wa kudumisha amani na utulivu duniani. Amesema katika dunia isiyo na utulivu, kuheshimiana ni njia ya kuishi kwa amani, na haki na usawa ni msingi wa usalama wa kudumu.

Rais Xi amesema China inapenda kushirikiana na nchi za kiarabu katika kuheshimu madhumuni na kanuni za Katiba ya Umoja wa Mataifa, kuheshimu chaguo la watu wa kila nchi, kuheshimu ukweli wa kihistoria uliopo, na kuchunguza njia za kutatua masuala zinazosaidia kulinda haki na usawa, na kutimiza amani na utulivu wa muda mrefu.

Pia amesema, China imeridhishwa na utekelezaji wa matunda yaliyopatikana kwenye Mkutano wa kwanza wa Wakuu wa China na Nchi za Kiarabu na inapenda kushirikiana na nchi za Kiarabu ili kuufanyia kazi uongozi wa kimkakati wa Mkutano huo na kuendelea kuhimiza maendeleo makubwa ya uhusiano kati ya China na nchi za Kiarabu.

Ameongeza kuwa, China itaandaa Mkutano wa pili wa Wakuu wa China na Nchi za Kiarabu nchini China mwaka 2026, ambao unatarajiwa kuwa hatua nyingine muhimu katika uhusiano wa pande hizo mbili.