Marais wa China na Misri wafanya mazungumzo Beijing
2024-05-30 09:13:25| CRI

Rais Xi Jinping wa China jana Jumatano alifanya mazungumzo na mwenzake wa Misri Abdel Fattah El-Sisi ambaye yuko ziarani mjini Beijing.

Rais Xi amesema Misri ni nchi ya kwanza ya kiarabu na ya Afrika kuanzisha uhusiano wa kibalozi na China miaka 68 iliyopita. Huu ni mwaka wa kumi tangu nchi hizo mbili zilipoanzisha uhusiano wa wenzi wa kimkakati wa pande zote. Uhusiano kati ya China na Misri umekuwa mfano hai wa mshikamano, uratibu na ushirikiano wa kunufaishana kati ya China na nchi za kiarabu, za Afrika, za kiislamu na zinazoendelea. Rais Xi amesema, China iko tayari kushirikiana na Misri katika kuimarisha kuaminiana, kukuza ushirikiano, kujenga jumuiya yenye mustakbali wa pamoja kati ya China na Misri, na kutoa mchango kwa amani, utulivu, maendeleo na ustawi wa kikanda na kimataifa.

Naye Rais El-Sisi amesisitiza kuwa Misri inashikilia kithabiti kanuni ya China moja, inaunga mkono kithabiti msimamo wa China kwenye masuala yanayohusiana na maslahi yake makuu likiwemo suala la Taiwan, Hong Kong, Xizang na haki za binadamu, na pia inaiunga mkono kithabiti China kukamilisha umoja wa kitaifa.

Rais El-Sisi ameongeza kuwa, mwaka huu wa ushirikiano kati ya Misri na China unatarajiwa kutoa fursa kwa nchi hizo mbili kuimarisha mawasiliano kati ya watu na kupanua ushirikiano kwenye nyanja mbalimbali ikiwemo TEHAMA, Akili Bandia (AI), nishati mpya, usalama wa chakula na mambo ya fedha.