Sudan yakataa wito wa Marekani kuhusu kurejea katika mazungumzo ya Jeddah
2024-05-30 09:25:52| CRI

Serikali ya Sudan imetangaza kukataa wito wa Marekani kuhusu kurejea katika jukwaa la mazungumzo ya Jeddah kati ya Jeshi la Sudan (SAF) na Kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF).

Bw. Malik Agar, naibu mwenyekiti wa Baraza la Mpito la Sudan amesema, Mwaliko uliotolewa na waziri wa mambo ya nje wa Marekani Bw. Anthony Blinken kwa Mwenyekiti wa Baraza la Mpito Bw. Abdel Fattah Al-Burhan kwenda kushiriki kwenye jukwaa la mazungumzo la Jeddah umeonesha dharau kwa Sudan na haukubaliki.

Bw. Agar amesema hayo wakati akihutubia mkutano wa kisiasa huko Bandari ya Sudan, mji mkuu wa jimbo la bahari ya Sham, mashariki mwa Sudan. Ameongeza kuwa Sudan haikubali na haitakubali kwenda Jeddah, sio kwa sababu haitaki amani, lakini kwa sababu amani inatakiwa kuwa na msingi. Hawatakubali bila ya kushauriwa.

Ameeleza kuwa kipindi hiki hakiwezi kukubali uingiliaji wa vyama vingine vya kisiasa vyenye ajenda tofauti, akisisitiza kuwa kipaumbele lazima kiwekwe katika kumaliza mapigano na kutimiza utulivu kabla ya kufikia makubaliano ya kitaifa kupitia mazungumzo kati ya Wasudan.