UM waonya juu ya hali mbaya ya lishe kwa wanawake na watoto wa Sudan
2024-05-31 08:39:20| CRI

Kutokana na tishio la njaa linaloongezeka nchini Sudan, mashirika ya Umoja wa Mataifa yameonya siku ya Alhamisi kwamba dalili zote zinaonesha kuzorota kwa hali ya lishe ya wanawake na watoto nchini humo.

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu ( OCHA), imesema Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF), Mpango wa Chakula Duniani na Shirika la Afya Duniani yametoa onyo hilo baada ya uchambuzi mpya wa hali ya sasa na inayotarajiwa katika msimu wa mvua unaoanza mwezi mmoja ujao.

OCHA imeendelea kusema kwamba, uhasama unaoendelea unazidisha vichochezi vya utapiamlo kwa watoto ambapo Darfur ya Kati, viwango vya utapiamlo mkali vinakadiriwa kuwa asilimia 15.6 miongoni mwa watoto walio chini ya miaka 5. Katika kambi ya wakimbizi ya Zamzam huko Darfur Kaskazini, kiwango hicho ni karibu asilimia 30.

Ofisi hiyo ilisema uchunguzi wa mwezi uliopita wa Madaktari Wasio na Mipaka katika kambi ya Zamzam uligundua kuwa zaidi ya theluthi moja ya wanawake wajawazito na wanaonyonyesha wana utapiamlo, na kubainisha kuwa wanajinyima mahitaji yao wenyewe ili kulisha watoto wao.