Ripoti iliyotolewa na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) imesema kiwango cha ukuaji wa uchumi wa Afrika kwa mwaka jana kilifikia asilimia 3.1, ikiwa ni chini ya asilimia 4.1 ya mwaka 2022.
Ripoti hiyo ya Mtazamo wa Uchumi wa Afrika mwaka 2024 iliyotolewa jana, imesema kiwango cha ukuaji wa uchumi wa Afrika kimeshuka kutokana na bei kubwa ya chakula na mafuta, mahitaji hafifu duniani yanayoleta shinikizo kwa biashara ya nje, mabadiliko ya tabianchi na majanga makubwa yanayosababishwa na hali ya hewa katika uzalishaji wa kilimo na upatikanaji wa nishati, pamoja na ukosefu wa utulivu wa kisiasa na mapigano katika baadhi ya nchi za Afrika.
Ripoti hiyo imesema, ingawa nchi za Afrika Kusini, Misri na Nigeria zilirekodi kiwango cha chini cha ukuaji wa uchumi, zaidi ya nusu ya nchi za Afrika zilirekodi ukuaji mkubwa wa uchumi kwa mwaka jana kuliko mwaka 2022, huku nchi za Burkina Faso, Djibouti, Eswatini, Libya, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Sudan zikirekodi ongezeko la pato la jumla la ndani (GDP) la zaidi ya asilimia mbili.