Safari ya meli kutoka mji wa Weihai, China kwenda visiwani Zanzibar, Tanzania ilizinduliwa rasmi jana Mei 29. Hii ni njia ya kwanza ya meli inayokwenda Afrika kufunguliwa kutoka bandari ya Weihai, na pia ni njia ya kwanza ya moja kwa moja ya baharini kutoka China kwenda bandari ya Zanzibar.
Saa nne asubuhi, meli ya Tina iliyobeba tani 830 za mizigo ikiwemo magari ya uhandisi na mabomba ya metali iliondoka polepole kwenye bandari ya Weihai mkoani Shandong, ikiashiria kufunguliwa rasmi kwa njia ya bahari ya kutoka forodha ya Weihai kwenda bara la Afrika. Meli hiyo inatarajiwa kuwasili bandari ya Zanzibar baada ya safari ya siku 30. Meneja mkuu wa kampuni ya mnyororo wa ugavi ya Huatan ya mji wa Weihai Bw. Liu Youzhi amesema kwa furaha kuwa, baada ya kuzinduliwa kwa safari hii, muda wa kusafirisha bidhaa zao kwenda Afrika utapungua kutoka siku zaidi ya 70 hadi kufikia siku 30 hivi, na gharama pia itapungua kwa nusu.
“Zamani mizigo ilifika bandari ya Weihai baada ya kuzunguka kupitia bandari ya Tianjin au bandari ya Shanghai, baada ya kufunguliwa kwa njia hii inayokwenda moja kwa moja nchini Tanzania, gharama za uchukuzi pia zitapungua kwa nusu.”
Baada ya njia ya baharini kutoka Weihai kwenda Zanzibar kuzinduliwa, itatoa huduma za uchukuzi hasa kwa makampuni ya China yanayofanya biashara barani Afrika kusafirisha mashine za uhandisi na vifaa vya ujenzi, ili kuhimiza bidhaa za viwandani kuuzwa Afrika. Forodha ya Weihai imechukua hatua mbalimbali za kurahisisha taratibu za kukagua na kupitisha mizigo, ili kuhakikisha meli na bidhaa zinapita kwenye forodha kwa ufanisi na kwa urahisi. Naibu maneja mkuu wa bandari ya Weihai Bw. Fang Yong anasema:
“Tumetumia mbinu maalumu ya huduma za maghala, na kutoa huduma za kituo-kimoja kwa makampuni kuweka oda, kuhifadhi bidhaa, kukagua mizigo, kupata kibali, na kupakia na kupakua mizigo.”
Huu ni mwaka wa 60 tangu China na Tanzania zianzishe uhusiano wa kibalozi, ikiwa ni matunda mapya ya ujenzi wa pamoja wa “Ukanda Mmoja, Njia Moja” kati ya nchi hizo mbili, uzinduzi wa njia ya baharini ya kutoka Weihai kwenda Zanzibar, utaweka daraja jipya kwa ajili ya kuhimiza muunganiko wa miundombinu, ufanisi wa biashara na maingiliano ya watu wa pande hizo mbili. Balozi wa Tanzania nchini China Bw. Khamisi Mussa Omar anasema,
“Ushirikiano kati ya China na Afrika una mustakbali mkubwa, tunapaswa kufanya juhudi kwa pamoja kuhakikisha pande zote mbili za njia hii zina bandari na miundombinu ya kiwango cha juu cha kimataifa, ili kuongeza uwezo wa kusafirisha mizigo, na kuiwezesha njia hii ya baharini kuleta manufaa makubwa zaidi ya kiuchumi.”
(Picha zatolewa na Shirika la Utangazaji la Weihai)