Tume Huru ya Uchaguzi nchini Afrika Kusini (IEC) imetangaza matokeo rasmi Jumapili jioni ikisema Chama tawala cha African National Congress (ANC) kimepata viti 159 kati ya 400 katika Bunge la Kitaifa kwenye uchaguzi mkuu wa 2024.
Kwa mujibu wa matokeo hayo chama kikuu cha upinzani, Democratic Alliance (DA), kimeshika nafasi ya pili kwa kupata viti 87 Bungeni, kikifuatiwa na Chama cha uMkhonto weSizwe (MK) chenye viti 58 na Economic Freedom Fighters (EFF) viti 39.
Zaidi ya Waafrika Kusini milioni 27 walishiriki katika uchaguzi wa kitaifa na majimbo uliofanyika Mei 29 ili kuchagua Bunge jipya la Kitaifa na mabunge ya majimbo. Hata hivyo mwishowe hakuna chama kilichopata kura nyingi katika Bunge la Kitaifa. ANC ilipata chini ya viti 200 ilichohitaji ili kudumisha utawala wake usiopingwa uliodumu kwa miaka 30 katika baraza la chini la bunge.
Kufuatia kutangazwa rasmi kwa matokeo ya uchaguzi siku ya Jumapili, Bunge jipya lililochaguliwa litakuwa na siku 14 kufanya kikao chake cha kwanza, ambapo wabunge watamchagua rais wa Afrika Kusini atakayeongoza miaka mitano ijayo kwa wingi wa kura.