Misri yasisitiza Israel kuondoka kwenye kivuko cha Rafah ili kuanza tena operesheni
2024-06-03 09:05:57| CRI

Kituo cha televisheni cha Al-Qahera News cha Misri kimeripoti kuwa Misri Jumapili ilisisitiza haja ya Israel kuondoka kwenye kivuko cha Rafah kilichoko upande wa Palestina ili kuanza tena operesheni yake,

Ikinukuu chanzo cha ngazi ya juu cha usalama Al-Qahera ilisema mkutano wa pande tatu uliohudhuriwa na wajumbe kutoka Misri, Marekani na Israel ulifanyika mjini Cairo, kujadili kufunguliwa tena kwa kivuko cha Rafah kati ya Misri na Ukanda wa Gaza.

Wakati wa mkutano huo, ujumbe wa Misri ulisema Israel inawajibika kikamilifu kwa kusitisha uingiaji wa vifaa vya misaada na misaada ya kibinadamu huko Gaza, na kutaka hatua za haraka zichukuliwe ili kupeleka angalau malori 350 ya misaada katika ukanda huo kila siku.

Wakati huohuo televisheni ya Kan inayomilikiwa na serikali ya Israel iliripoti Jumapili kuwa Israel imetoa ridhaa yake kwa Hamas kupitia Qatar juu ya masharti mengi ya maelezo yalioandaliwa na Hamas kwa ajili ya kuachiliwa kwa mateka wa Israeli wanaoshikiliwa katika Ukanda wa Gaza.