Wanafunzi wa Uganda wahimizwa kujifunza lugha ya Kichina ili kuwa na matarajio mazuri ya kazi
2024-06-04 09:45:16| CRI

Mtaalamu msaidizi wa mtaala wa lugha za kigeni katika Kituo cha Taifa cha Kukuza Mtaala nchini Uganda (NCDC) Hilda Ayebare, amewahimiza wanafunzi wa nchi hiyo kuendelea kujifunza lugha ya Kichina.

Akiongea kwenye fainali za Uganda za shindano la umahiri wa Kichina zilizofanyika Jumapili katika Chuo cha Kyambogo cha mjini Kampala, amesema wanafunzi wao wote wanapaswa kujifunza Kichina kwa sababu kazi au fursa nyingi huja wakati unajua angalau lugha mbili za kigeni. Amebainisha kuwa tayari wameanzisha ufundishaji wa lugha ya Kichina katika mtaala wao, katika shule za sekondari ya chini na ya juu kote nchini Uganda tangu 2020.

Naye mwambata mshauri wa Ubalozi wa China nchini Uganda Fan Xuecheng, alisema mashindano ya "Daraja la Kichina" yaliyozinduliwa miaka 23 iliyopita, yamekuwa jukwaa la mawasiliano baina ya wanafunzi wa lugha ya Kichina duniani kote, na kusaidia watu wengi zaidi kuelewa kwa kina utamaduni wa China na China kwa ujumla.