Tanzania yaimarisha ushirikiano na China katika elimu ya ufundi stadi
2024-06-04 09:45:46| CRI

Tanzania Jumatatu iliahidi kuimarisha ushirikiano na China katika kuendeleza elimu na mafunzo ya ufundi stadi (TVET) ili kukidhi viwango vya ndani na kimataifa kwa wahitimu.

Akizungumza katika Semina ya Pili ya China na Afrika ya Ubadilishanaji wa Kitaaluma ya TVET jijini Dar es Salaam, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, James Mdoe, alisema China ni nchi ya kupigiwa mfano yenye mifumo imara ya TVET ambayo imechangia kwa kiasi kikubwa maendeleo ya haraka ya uchumi wa Tanzania.

Mdoe alisema Tanzania itanufaika kwa kuanzisha ushirikiano na vyuo vya TVET vya China ili kuboresha ubora wa mafunzo. Ameongeza kuwa ili kuendeleza uwekezaji nchini kunahitaji nguvu kazi yenye ujuzi, ikiwemo miradi ya kimkakati.

Naye Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET), Adolf Rutayuga amesema semina hiyo inalenga kuimarisha ushirikiano wa TVET kati ya Tanzania na China, kuboresha elimu ili kuzalisha wahitimu wenye ujuzi na uwezo ambao watakidhi matakwa ya soko la ajira la kitaifa na kimataifa.