Serikali ya Tanzania imesema katika kipindi cha mwaka 2024/2025, imepanga kutumia Sh bilioni 30 kuimarisha huduma za watoto wachanga katika hospitali 100 nchini humo.
Hayo yamesemwa jana na Naibu Waziri wa Afya wa Tanzania, Dk Godwin Mollel katika kikao cha Bunge kinachoendelea mjini Dodoma. Amesema katika kipindi cha mwaka 2024/2025, serikali imepanga kutumia fedha hizo kuimarisha huduma za watoto wachanga katika hospitali 100 kwa kujenga wodi maalum (NCU) za watoto wachanga, watoto njiti, na ununuzi na usambazaji wa vifaa tiba ikiwemo mashine za kuwasaidia watoto wachanga njiti kupumua.