Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Zanzibar, Dkt. Mzee Suleiman Mndewa amewataka wataalamu wa masuala ya Posta barani Afrika kutumia vyema maendeleo ya teknolojia katika kuwezesha sekta hiyo kufungua fursa za kiuchumi na kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi katika nchi hizo.
Dkt. Mndewa amesema hayo jana mkoani Arusha wakati akifungua Vikao vya Kamati za wataalamu wa masuala ya Posta kutoka nchi wanachama wa Umoja wa Posta Afrika (PAPU), ikiwa ni vikao vya utangulizi kabla ya Mkutano wa 42 wa Baraza la Utawala la PAPU litakalofanyika Juni 11 hadi 12 jijini humo.
Amesema ili nchi za Afrika ziweze kufanikiwa zaidi katika masuala ya Posta na kuendana na kasi ya ukuaji wa biashara katika mtandao, ni wajibu wao kwa pamoja kama nchi wanachama kuhakikisha kila mmoja anashiriki katika uchumi wa kidigitali.