Umoja wa Afrika (AU) Jumatatu ulitahadharisha kuhusu athari za kuongezeka kwa migogoro na mabadiliko ya serikali kinyume na katiba, ambayo inatishia misingi ya demokrasia na usalama wa nchi za Afrika.
Kauli hiyo ilitolewa Jumatatu na mkurugenzi wa usimamizi wa migogoro ndani ya Idara ya Masuala ya Kisiasa, Amani na Usalama ya Kamisheni ya AU, Alhaji Sarjoh Bah, wakati akihutubia mkutano wenye kauli mbiu ya amani na usalama wa barani humo, kwenye makao makuu ya AU mjini Ethiopia Addis Ababa.
Bah amesema Afrika, kwa bahati mbaya, imeshuhudia kuongezeka kwa migogoro katika maeneo kama vile Pembe ya Afrika, Sahel, na Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Mkurugenzi huyo alisisitiza kwamba matukio kama hayo husababisha ombwe ambalo linatumiwa na makundi ya kigaidi na watu wenye msimamo mkali, huku wahusika wa nje wakizidi kuyumbisha jamii na kuzuia kupiga hatua kuelekea amani endelevu.