Naibu msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, Bw. Farhan Haq amesema askari wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa wanashika doria kulinda watu laki moja na elfu hamsini waliokimbia makazi yao kutokana na mapigano katika mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Bw. Farhan Haq amesema kuwa Tume ya kulinda amani ya Umoja wa Mataifa nchini DRC (MONUSCO) imeripoti mapigano makali mfululizo kati ya kundi la waasi la M23 na wanajeshi wa DRC kusini mwa Kanyabayonga katika eneo la Rutshuru, Kivu Kaskazini yalitokea wikiendi.
Mapigano hayo yamesababisha raia kuhama makazi yao kuelekea Kayna, Miriki na Kirumba, huku wengine wakifika Lubero na Butembo. Ili kukabiliana na hali hiyo, walinda amani na wanajeshi wa Kongo kwa uratibu wameweka doria karibu na Kanyabayonga kuwasaidia wakimbizi hao. Wafanya doria hao wametoa huduma za matibabu na kuwasindikiza watu katika maeneo salama, na kwamba Tume hiyo inadumisha uwepo wake huko.