Wavuvi katika Wilaya ya Kilwa Mkoa wa Lindi, kusini mwa Tanzania, wameeleza matumaini makubwa juu ya ujenzi wa bandari wakisema itawasaidia kuhifadhi samaki wao.
Akiongea na shirika la habari la China Xinhua, mvuvi Sudi Saidi amesema tangu Wachina waanze kujenga bandari ya uvuvi, sasa hana wasiwasi tena. Pia amesema bandari hiyo iliyojengwa na Kampuni ya Uhandisi wa Bandari ya China (CHEC) itakuza biashara yake ya uvuvi kwa njia mbalimbali.
Saidi alibainisha kuwa baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa bandari hiyo Septemba 2023, hali ya uchumi wa Wilaya ya Kilwa ilianza kubadilika na kuwa bora, ambapo hivi sasa imekuwa na shughuli nyingi kufuatia ujenzi wa bandari hiyo. Mvuvi mwingine anayejulikana kwa jina la Ahmad Saidi Bakari alisema bandari hiyo mpya ya uvuvi imenufaisha eneo hilo ikiwa ni pamoja na kuajiri wananchi.
Meneja wa Idara ya Mradi wa CHEC Tanzania, Bian Liang, alisema ujenzi wa bandari ya uvuvi unakadiriwa kufikia asilimia 65 na kulingana na maendeleo ya utekelezaji wa mradi, inatazamiwa kuwa mwishoni mwa Oktoba 2024, gati na miundombinu yake mingi itakamilika.