Soko la Pamoja la Mashariki na Kusini mwa Afrika (COMESA), jumuiya ya kiuchumi ya kikanda, Jumanne ilizindua mradi unaolenga kuongeza kasi ya upatikanaji wa nishati katika kanda za mashariki na kusini mwa Afrika.
Mradi huo wa Kuharakisha Upatikanaji wa Nishati Endelevu na Safi unalenga kuleta muunganisho mpya wa umeme kwa watu milioni 100 katika kipindi cha miaka saba ijayo. Pia unalenga kupanua muunganisho wa umeme wa gridi na nje ya gridi ya taifa, kuleta suluhu za nishati mbadala, teknolojia safi ya kupikia na mafuta.
Katika uzinduzi huo uliofanyika mjini Lusaka, Zambia, Katibu Mkuu wa COMESA Chileshe Mpundu Kapwepwe alisema nchi za Afrika zinahitaji uwekezaji mkubwa ili kutatua changamoto zao za nishati. Alisema kwa mujibu wa makadirio ya Benki ya Maendeleo ya Afrika, takriban dola za Kimarekani bilioni 35 zinahitajika kufikia upatikanaji wa nishati kwa wote barani Afrika ifikapo mwaka 2030.
Mradi huu umetengewa dola bilioni 5 na Jumuiya ya Maendeleo ya Kimataifa na unalenga kutumia dola bilioni 10 za ziada kutoka kwa washirika wengine kwa ajili ya uwekezaji katika gridi ya taifa na usambazaji wa nishati mbadala.