Gavana wa Jiji la Nairobi nchini Kenya, Johnson Sakaja ameanzisha kikosi kipya kilichopewa jukumu la kukagua upya miradi ya ujenzi iliyoidhinishwa kwa muda wa miaka miwili iliyopita, hatua inayolenga kuhakikisha kuwa miradi au majengo hayo yanakidhi viwango vilivyowekwa.
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari iliyotolewa jana jijini Nairobi, Gavana huyo amesema tayari serikali ya Kaunti ya Jiji hilo kupitia ofisi ya kaimu Katibu wa Kaunti imewaandikia wadau husika na kuwataka kuwasilisha majina ya wataalamu na wawakilishi ambao watakuwa sehemu ya kikosikazi cha ukaguzi huo.
Amesema wajumbe wa kikosikazi hicho watakutana tarehe 12 mwezi huu ili kuanza ukaguzi huo, na wamepewa siku 60 za kukamilisha kazi hiyo na kuwasilisha ripoti kwa ajili ya utekelezaji.