Watu wanane wafariki kwa sumu ya methanol nchini Morocco
2024-06-06 10:00:01| cri

Watu wanane wamefariki na wengine 114 wamelazwa hospitali baada ya kunywa pombe ya kienyeji iliyotengenezwa kwa kutumia methanol nchini Morocco.

Shirika la Habari la nchini humo MAP limesema tukio hilo limetokea katika mji wa Sidi Allah El Tazi katika mkoa wa Kenitra, ambapo watu 114 katika mji huo wenye idadi ya watu zaidi kidogo ya 3,100, wanasumbuliwa na athari za sumu ya methanol kuanzia jumatatu wiki hii hadi jana.

Habari zinasema rasilimali zote muhimu zimeandaliwa kupokea kesi mpya katika taasisi za afya mkoani humo, huku uratibu wa karibu ukianzishwa kati ya mamlaka za huko ili kutambua kesi yoyote inayoweza kufikishwa katika vituo vya afya na hospitali.