Chama tawala nchini Afrika Kusini cha African National Congress (ANC) kimesema Jumatano kwamba kimeanza mazungumzo na vyama vikuu vya kisiasa nchini humo ili kuunda serikali ya umoja wa kitaifa baada ya kupoteza viti vingi katika Bunge la Taifa katika uchaguzi mkuu uliomalizika hivi karibuni.
ANC kimepata viti 159 kati ya 400 vya Bunge, huku Democratic Alliance (DA) kikishika nafasi ya pili kwa kupata viti 87, kikifuatiwa na Chama cha Umkhonto weSizwe (MK) chenye viti 58 na Economic Freedom Fighters (EFF) viti 39. .
Katika taarifa yake kufuatia Mkutano wake wa Taifa wa Kamati ya Kazi, ANC ilisema matokeo ya uchaguzi wa kitaifa na majimbo wa 2024 yanaonesha kuwa Waafrika Kusini wanataka vyama vyote kufanya kazi kwa pamoja, kwa sababu hakuna chama kilichopata wingi wa kura ili kuunda serikali pekee katika ngazi ya kitaifa, na kuongeza kuwa hadi sasa kimekutana na vyama vya siasa vikiwemo DA na EFF, huku kikijaribu kukifia Chama cha MK mara kwa mara ili kukutana kwa mazungumzo, lakini hakijafanikiwa.