Wanafunzi 500 kupewa nafasi vyuo vya watu wenye ulemavu nchini Tanzania
2024-06-06 10:00:28| cri

Serikali ya Tanzania imesema mwaka 2024/2025 imepanga kudahili wanafunzi 1500 kupitia vyuo vyake vya watu wenye ulemavu, kati yao wasio na ulemavu ni 500 sawa na asilimia 30 ya wanafunzi wote.

Akizungumza katika kikao cha Bunge kinachoendelea katika mji mkuu wa Tanzania, Dodoma, Naibu Waziri Maendeleo ya Jamii, Jinsi, Wanawake na Makundi Maalum, Mwanaidi Ali Khamis, amesema serikali imeandaa Mwongozo wa Utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Elimu Jumuishi 2022-2028 wa Oktoba 2022.

Pia amesema serikali inatekeleza Mpango Mkakati wa Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu 2023/24 – 2025/26, ambao pamoja na mambo mengine unahusu suala la elimu na ujuzi kwa kuzingatia ujumuishaji wa watu wenye na wasio na ulemavu katika maeneo ya kujifunza.