Rais wa China ajibu barua aliyoandikiwa na mkuu wa Chuo Kikuu cha Kean cha Marekani
2024-06-06 15:09:19| cri

Hivi karibuni Rais Xi Jinping wa China amejibu barua aliyoandikiwa na mkuu wa Chuo Kikuu cha Kean cha Marekani Bw. Lamont Repollet, akivihamasisha vyuo vikuu vya China na Marekani viimarishe mawasiliano na ushirikiano, na kutoa mchango wao katika kuhimiza urafiki kati ya nchi hizo mbili.

Rais Xi amesema, mwaka 2006 alipokuwa katika Chuo Kikuu cha Kean nchini Marekani, alishuhudia kusainiwa kwa makubaliano ya kuanzisha chuo kikuu cha Wenzhou-Kean, na kutokana na juhudi za pamoja za pande mbili, chuo kikuu cha Wenzhou-Kean kimekuwa mfano wa ushirikiano wa elimu kati ya China na Marekani.

Rais Xi amebainisha kuwa, uhusiano kati ya China na Marekani unahusisha maslahi ya watu wa nchi hizo mbili na mustakbali na hatma ya binadamu. Mawasiliano na ushirikiano wa kielimu vinasaidia kuhimiza maelewano kati ya watu, haswa vijana wa nchi hizo mbili, na ni mradi wa siku zijazo wa kukuza uhusiano wa China na Marekani. Rais Xi ameeleza matumaini yake kwamba vyuo vikuu vya China na Marekani vitaimarisha mawasiliano na ushirikiano kwa njia mbalimbali, kuandaa wajumbe vijana wanaozifahamu China na Marekani, na kujenga madaraja mengi zaidi ya urafiki kati ya nchi hizo mbili.