Wizara ya Afya na Huduma za Jamii nchini Namibia imesema, mlipuko wa surua umethibitishwa katika mkoa wa Erongo, katikati-magharibi mwa nchi hiyo.
Mkurugenzi Mkuu wa Wizara hiyo, Ben Nangombe amesema, mlipuko huo ulioanza mwezi Januari mwaka huu, umeshuhudia jumla ya kesi 93 zinazoshukiwa kuwa na maambukizi. Amesema watu waliothibitishwa kuwa na maambukizi wamepona ama wanaendelea vizuri, na kwamba hakuna wagonjwa waliolazwa hospitalini ama kufariki.
Ili kukabiliana na mlipuko huo, Wizara hiyo imeanzisha timu ya mwitikio katika mkoa huo na inawafuatilia na kuwapima watu waliowasiliana kwa karibu na wagonjwa, na kuongeza kuwa elimu ya afya pia inatolewa kwa wanafunzi, waalimu na jamii kwa ujumla, huku mipango ya kutoa chanjo ya ziada ikiendelea katika wilaya iliyoathiriwa zaidi.