UNECA na washirika wake waungana kukuza maendeleo ya magari ya umeme na teknolojia za kuhifadhi nishati barani Afrika
2024-06-07 08:47:08| CRI

Tume ya Uchumi ya Umoja wa Mataifa katika Afrika (UNECA) ikishirikiana na Shirika la Maendeleo na Ushirikiano wa Muunganisho wa Nishati Duniani (GEIDCO), na Chama cha Mashirika ya Umeme Afrika (APUA), wamezindua mpango wa kukuza maendeleo ya magari ya umeme (EVs) na teknolojia ya kuhifadhi nishati barani Afrika.

Kwenye taarifa yake UNECA ilisema mpango huo, unatoa mafunzo kuhusu magari ya umeme na teknolojia ya kuhifadhi nishati kwa maendeleo endelevu ya Afrika, yanayoungwa mkono na makampuni ya magari ya umeme ya China. Mafunzo hayo yanayoanzia tarehe 4-14 Juni, yameshirikisha zaidi ya watu 140 kutoka nchi 25 za Afrika, wanaotoka wizara za uchukuzi na nishati, tume za nishati, makampuni ya umeme, na wasomi, pamoja na mashirika mengine ya maendeleo ya Afrika.

Wakati huohuo mtendaji mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati ya Zimbabwe (ZERA), Edington Mazambani amepongeza kuongezeka kwa idadi ya miradi ya nishati mbadala nchini humo inayofadhiliwa na China, akisema imesaidia kuleta utulivu na kupunguza shinikizo kwenye gridi ya umeme nchini humo. Amesema makampuni kadhaa ya uchimbaji madini ya China yameanzisha mitambo ya nishati mbadala ili kuhakikisha upatikanaji wa nishati katika shughuli zao za uchimbaji madini.