Wataalamu wa Umoja wa Mataifa wamesema Afrika inakabiliwa na changamoto nyingi katika sekta yake ya madini, huku ukosefu wa mfumo wa ramani za kijiografia likiwa ni tatizo kubwa linalozuia bara hilo kutumia vizuri utajiri mkubwa wa madini yaliyomo.
Timu ya wataalamu kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la Biashara na Maendeleo (UNCTAD) imesema jumamosi kuwa, Afrika inashikilia karibu 1/5 ya hifadhi ya metali ambayo ni muhimu sana kwa nishati ikiwemo metali zinazohitajika katika utengenezaji wa magari ya umeme.
Akihojiwa na Shirka la Habari la China Xinhua, Mkuu wa Kitengo cha Utafiti wa Bishara na Tathmini katika Shirika hilo Clovis Freire amesema, Afrika ina hifadhi kubwa zaidi ya madini duniani lakini inakosa mfumo wa ramani wa kijiografia, ambao unaweza kuvumbua kiasi kikubwa cha rasilimali.
Amesema kuna haja ya ukaguzi wa kina wa kijiografia na ufundi wa kisasa katika utafiti ili kutambua madini yasiyojulikana ama hifadhi za madini ambazo hazijagunduliwa, hatua inayoweza kutoa fursa kubwa kwa aina mpya za uchimbaji wa madini katika bara hilo.