Katibu Mkuu mpya wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) Veronica Mueni Nduva, amesema vipaumbele vyake ni pamoja na kuimarisha maingiliano ya kiuchumi yanayochochea uvumbuzi, ujasiriamali na utoaji wa nafasi ya ajira pamoja na amani na usalama.
Taarifa iliyotolewa na Makao Makuu ya Jumuiya hiyo yaliyoko Arusha, Tanzania imesema, Bi. Nduva alitoa vipaumbele hivyo baada ya kuapishwa katika Mkutano wa 23 wa Wakuu wa EAC uliofanyika Ijumaa iliyopita.
Alipohojiwa na Shirika la Habari la China Xinhua, Bi. Nduva amesema muhula wake utajikita zaidi katika kuboresha maingiliano ya kina na maendeleo ya watu wa Afrika Mashariki. Pia amesema, maendeleo ya kisasa ya kijamii yatapewa umuhimu mkubwa kwake, huku nafasi kubwa ikitolewa katika kuwawezesha wanawake na vijana, ambao ni msingi wa jamii katika kanda hiyo.
Bi. Nduva anachukua nafasi ya Peter Mathuki ambae amepewa nafasi nyingine na serikali ya Kenya.