Juhudi za kutokomeza ndoa za utotoni
2024-06-14 08:20:31| CRI

Tukumbuke kwamba wiki iliyopita tulisema kwamba kuelekea Siku ya Mtoto wa Afrika ambayo ni kesho tarehe 16 tutazungumzia madhila wanayokumbana nayo watoto. Wiki iliyopita tulijadili kwa kina kuhusu mila potofu zinazotekelezwa kwa watoto wa kike. Na leo tutaangalia ndoa za utotoni. Sasa licha ya kampeni zinazoendelea za kutokomoza kabisa ndoa za utotoni, baadhi ya wazazi na walezi katika maeneo mbalimbali bado wanaendeleza vitendo hivi vya kuwaoza watoto wa kike wakiwa bado wana umri mdogo kabisa. Wasichana hawa wanajikuta wakilazimishwa kuolewa kabla ya kutimiza miaka 18.

Hata hivyo kwa upande wa pili kampeni hizi zinaonekana kuzaa matunda ingawa sio mengi. Ripoti ya shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) iliyotolewa mwaka jana imeeleza kwamba vitendo vya ndoa za utotoni vimeendelea kupungua duniani ingawa kasi yake ya si kutosha kuweza kufikia lengo la kutokomeza ndoa za utotoni ifikapo mwaka 2030, kama inavyoelekezwa kwenye Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa.

Pamoja na kupungua huko kwa vitendo vya kuozesha watoto wakiwa wadogo, UNICEF inasema India imeendelea kuwa na idadi kubwa zaidi duniani ya watoto wanaoolewa mapema. Ripoti hiyo pia inaeleza kuwa baadhi ya maeneo duniani yameshudia kupungua kwa vitendo vya ndoa katika umri mdogo, lakini mataifa mengine yamekwama hasa zaidi katika eneo la Afŕika Magharibi na Kati, kanda inayotajwa kuwa yenye matukio mengi zaidi ya ndoa za utotoni.

Nchi nyingi katika kanda hii, hasa zile za Sahel, zimekumbwa na migogoro inayoendelea ambayo inazidisha mazingira magumu kwa wasichana. Hivyo kama tulivyotangulia kusema leo katika kipindi cha Ukumbi wa Wanawake tutaangalia juhudi zinazoendelea za kutokomeza ndoa za utotoni.