Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa jana lilipitisha azimio namba 2735, likitoa wito wa kusitisha vita mara moja na kwa pande zote katika Ukanda wa Gaza ili kumaliza mzozo wa Palestina na Israel uliodumu kwa miezi minane haraka iwezekanavyo.
Azimio hilo limeungwa mkono na nchi wajumbe wa kudumu 14 kati ya 15 wa Baraza hilo, huku Russia ikijizuia. Azimio hilo linaitaka Israel na Kundi la Hamas kutekeleza kikamilifu azimio hilo "bila kuchelewa na bila masharti, na kusisitiza kuwa, Baraza la Usalama linakataa jaribio lolote la mabadiliko ya kidemografia au kimaeneo katika Ukanda wa Gaza, huku likisisitiza dhamira yake thabiti ya suluhisho la serikali mbili.
Ikulu ya Rais wa Palestina jana ilitoa taarifa na kusema, kupitishwa azimio hilo ni mwelekeo sahihi na itasaidia kusitisha vita vya sasa dhidi ya wananchi wa Ukanda wa Gaza.
Kundi la Hamas pia limetoa taarifa siku hiyo, likikaribisha kupitishwa kwa azimio hilo na kueleza nia yake ya kushirikiana na wapatanishi hao kufanya mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja kuhusu utekelezaji wa kanuni zinazoendana na matakwa ya watu wa Gaza na kundi hilo.