Shirika la Kuhudumia Watoto wa Umoja wa Mataifa (UNICEF) limesema karibu watoto milioni 400 duniani wenye umri wa chini ya miaka mitano wanakabiliwa na athari za kisaikolojia ama adhabu za kivitendo majumbani kwao.
Takwimu zilizotolewa na UNICEF katika maadhimisho ya kwanza ya Siku ya Kimataifa ya Michezo zimeonyesha kuwa, watoto milioni 330 wanaadhibiwa kwa njia za kimwili.
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo Catherine Russell amesema, watoto wanakabiliwa na udhalilishaji wa kimwili na maneno wakiwa majumbani, ama wanapokosa huduma za kijamii na kihisia kutoka kwa wapendwa wao, jambo linaloweza kuondoa hisia zao za kujithamini na maendeleo yao.
Ili kuhakikisha watoto wanakua wakihisi usalama na kupendwa, Shirika hilo limetoa wito kwa serikali kuimarisha juhudi na uwekezaji katika ulinzi kwa kuboresha mifumo ya kisheria na kisera inayozuia na kuondoa aina zote za uhalifu dhidi ya watoto majumbani kwao, kuzuia uhalifu wa kifamilia, na kuongeza nafasi za kujifunza na elimu kwa watoto.