Rais wa China ahutubia Ufunguzi wa Maadhimisho ya Miaka 60 ya Mkutano wa UNCTAD
2024-06-13 08:44:04| CRI

Rais Xi Jinping wa China ametoa hotuba kwa njia ya video kwa ufunguzi wa Maadhimisho ya Miaka 60 ya Mkutano wa Biashara na Maendeleo ya Umoja wa Mataifa (UNCTAD) uliofanyika jana jumatano.

Katika hotuba hiyo, rais Xi amesema, katika miaka 60 iliyopita tangu kuanzishwa kwake, mkutano huo umekuwa ukifuata kanuni ya kutafuta ustawi wa pamoja, kuhimiza ushirikiano na mazungumzo ya Kusini na Kusini, kuhimiza ujenzi wa utaratibu mpya wa uchumi wa kimataifa, na kutoa mchango muhimu kwa biashara na maendeleo duniani.

Pia amesisitiza kuwa China siku zote ni moja kati ya nchi za Dunia ya Kusini, na daima itanufaisha nchi zinazoendelea. Amesema katika siku za usoni, China itaongeza uagizaji wa bidhaa kutoka nchi nyingine duniani, kuimarisha biashara, uwekezaji na ushirikiano, ili kuchangia katika utekelezaji wa Ajenda ya Mwaka 2030 ya Maendeleo Endelevu.