Nchi za Afrika Mashariki zimezindua mfumo wa kina utakaowaongoza wadau wa sekta ya afya katika kutokomeza ugonjwa wa usubi.
Taasisi ya utafiti ya Madawa na Magonjwa Yasiyopewa umuhimu (DSDi) imesema katika taarifa yake iliyotolewa jijini Nairobi, Kenya, kwamba eneo la Afrika Mashariki lilichukua asilimia 70 ya kesi za usubi duniani mwaka 2022, na nusu ya kesi hizo ziliwakuta watoto wenye umri wa chini ya miaka 15.
Ugonjwa huo ambao haujapewa kipaumbele kinachotakiwa kama moja ya magonjwa ya kitropiki unasababishwa na vimelea na dalili zake ni pamoja na homa, kupungua uzito, kupanuka kwa ini na bandama.
Mwongozo huo umeandaliwa na Shirika la Afya Duniani na wenzi wake ikiwemo Taasisi ya DNDi na mawaziri wa afya katika kanda hiyo, na umetoa maeneo matano ya kimkakati, ambayo ni pamoja na kutambua mapema na kutibu ugonjwa huo, kutoa elimu, na utafiti.