Vikosi vya ulinzi vya Afrika Mashariki vyaanza mazoezi ya kijeshi nchini Rwanda
2024-06-14 08:42:31| CRI

Maofisa 1,000 wa jeshi la ulinzi na polisi kutoka nchi nne wenzi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) wameanza mazoezi ya kijeshi ya wiki mbili jana Alhamis mashariki mwa Rwanda.

Zoezi hilo lililopewa jina la Ushirikiano Imara, lilizinduliwa katika Chuo cha Kijeshi cha Rwanda kilichoko eneo la Gako, katika wilaya ya Bugesera chini ya kaulimbiu “Kuimarisha maingiliano katika sekta ya usalama na kuboresha maslahi ya pamoja kuendana na utulivu na usalama wa kanda ya Afrika Mashariki.”

Akizungumza katika hafla ya ufunguzi wa mazoezi hayo, Waziri wa Ulinzi wa Rwanda Juvenal Marizamunda ametoa wito wa juhudi za uratibu ndani ya kanda hiyo ili kukabiliana na changamoto za sasa za usalama. Amesema mazoezi hayo yanatoa fursa ya kuboresha uhusiano na maingiliano ya operesheni, kuwezesha kanda hiyo kukabiliana kwa ufanisi na matishio yanayoweza kutokea.

Washiriki wa mazoezi hayo wanatokea Kenya, Tanzania, Uganda na Rwanda.