Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa (UNICEF) limesema uwekezaji mkubwa katika elimu ya msingi kwa watoto barani Afrika unahitajika ili kusaidia bara hilo kutimiza ajenda yake ya muda mrefu ya mageuzi.
UNICEF imesema hayo siku chache kabla ya kuadhimishwa kwa Siku ya Mtoto wa Afrika Juni 16.
Shirika hilo limesema, fedha zinazotengwa kwa ajili ya sekta ya elimu katika bara la Afrika bado ni kidogo, na kuongeza kuwa, nchi moja kati ya tano zimetenga asilimia 20 ya bajeti zao kuboresha ujuzi wa kimsingi kwa watoto wao.
Mkurugenzi wa UNICEF kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika, Etleza Kadili, amesema katika taarifa yake iliyotolewa mjini Nairobi, Kenya, jana, kuwa ili kuhakikisha ustawi wa Afrika, ni lazima kuonyesha nia halisi ya kubadili ahadi kuwa vitendo halisi ili watoto waweze kupata misingi muhimu ya elimu ya msingi itakayowawezesha kuendelea katika elimu za juu na kutimiza uwezo wao kamili.
Kaulimbiu ya Siku ya Mtoto wa Afrika mwaka huu ni “Elimu kwa watoto wote wa Afrika: Wakati ni Huu,” na inasisitiza haja ya dharura ya elimu kwa watoto wote katika bara hilo.