Kenya yatangaza bajeti iliyoweka rekodi ili kuendeleza ukuaji wa uchumi
2024-06-14 10:31:23| cri

Kenya imewasilisha bajeti yake ya shilingi trilioni 3.9 (kama dola bilioni 30 za Kimarekani) kwa mwaka wa fedha wa 2024/2025, ikilenga kudumisha ukuaji wa uchumi. Waziri wa fedha na mipango ya uchumi wa Kenya Bw. Njuguna Ndung'u, amesema hayo wakati akiwasilisha taarifa ya bajeti mbele ya Bunge mjini Nairobi, na kusema serikali inalenga kukuza ukuaji wa uchumi baada ya kuimarika tena mwaka 2023.

Bw. Ndung’u amesema uchumi wa Kenya kwa sasa unaondokana na misukosuko hasi, ambayo baadhi ina athari za kimuundo katika shughuli za kiuchumi. Amesema kuimarika kwa uchumi ni dhahiri, ambapo ukuaji wa pato la taifa ulifikia asilimia 5.6 mwaka 2023, kutoka asilimia 4.9 mwaka 2022. Ukuaji huo ulichangiwa kwa kiasi kikubwa na ukuaji wa shughuli za kilimo, kutokana na kuimarika kwa hali ya hewa, na uwepo pembejeo za ruzuku kwa wakulima.