Timu ya China yaandaa mafunzo kuhusu uhifadhi wa urithi wa kiutamaduni kwa wanafunzi wa Afghanistan
2024-06-17 08:25:44| CRI

Mafunzo maalum yanayolenga kuhimiza uhifadhi wa urithi wa kiutamaduni kwa wanafunzi wa shule ya msingi nchini Afghanistan yalifanyika Jumapili mkoani Bamiyan, katikati ya nchi hiyo.

Mafunzo hayo yaliandaliwa na timu ya watu sita inayoundwa na wanaakiolojia na wataalamu wa urithi wa kiutamaduni wa China, pamoja na wataalam na maofisa wa Afghanistan, kwenye maeneo ya Sanamu Kubwa ya Budhaa na Shahr-e Gholghola yaliyoko katika bonde la Bamiyan, ambayo yote yaliorodheshwa na Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) kuwa Urithi wa Dunia.

Kwenye mafunzo hayo, wanafunzi wa Afghanistan walifundishwa kuhusu hali ya sasa ya uhifadhi wa urithi wa kiutamaduni huko Bamiyan, ustadi wa kiutendaji unaohitajika katika uhifadhi wa urithi, na historia ya mawasiliano ya kiutamaduni kati ya China na Afghanistan kuhusu Njia ya Hariri ya Kale.