Nyagatare: Ugonjwa wa miguu na midomo waikumba Tabagwe huku ikiwekwa karantini
2024-06-17 10:47:11| cri

Bodi ya Kilimo na Rasilimali ya Wanyama ya Rwanda (RAB) imeweka karantini ya mifugo huko Nyagatare, hasa katika kitongoji cha Tabagwe, kufuatia mlipuko wa ugonjwa wa miguu na midomo.

Kwa mujibu wa RAB, karantini hiyo inalenga kuzuia kuenea kwa ugonjwa huo katika maeneo mengine na kulinda idadi ya mifugo kote nchini.

Maafisa wa RAB pia wanasema wanafanya kazi kudhibiti na kutokomeza ugonjwa huo katika eneo lililoathiriwa.

Dk. Solange Uwituze, Naibu Mkurugenzi Mkuu anayesimamia Rasilimali za Wanyama katika RAB alisema hadi sasa, kesi 118 zimeripotiwa. Wanyama waliopatikana na virusi wameondolewa shambani mara moja.

Wakulima wa Tabagwe wametakiwa kuripoti tukio lolote linaloshukiwa kuwa ni la ugonjwa huo kwa maafisa wa mifugo katika ngazi ya kitongoji ili kuhakikisha uingiliaji kati na udhibiti wa hali hiyo kwa wakati, pamoja na kuwaweka mifugo katika zizi na mashamba, na mara kwa mara kutumbukiza kwenye maji mifugo yao.