Bara la Afrika lina idadi kubwa ya vijana, na ustawi wa vijana unahusiana na mustakabali wa Afrika. China inaweka mkazo mkubwa katika kuandaa wataalamu vijana kwa Afrika. Chini ya pendekezo la ujenzi wa pamoja wa Ukanda Mmoja, Njia Moja, na Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC), China inaunga mkono vijana bora kusoma nchini China, kuwasaidia vijana kurudi nchini kwao baada ya kumaliza masomo, ili kuchangia maendeleo ya kiuchumi na kijamii ya huko.
Msomi kutoka nchini Eritrea Dr. Henok Neguse Negash anaona kuwa, katika miaka ya hivi karibuni, kutokana na uongozi wa mifumo ya ushirikiano ya Ukanda Mmoja, Njia Moja, na FOCAC, mawasiliano ya wanafunzi kati ya China na Afrika yanaongezeka kwa kasi, hali ambayo inazinufaisha pande zote mbili. Anaamini huo ni ushirikiano wa kunufaishana na unatakiwa kudumishwa.
Pia amesema elimu ni moja ya nguzo muhimu za maendeleo ya kiuchumi kwa nchi zote, na ukuaji wa uchumi utaweza kuhakikishwa ikiwa idadi kubwa ya watu wa nchi husika wamepata elimu. Mawasiliano kati ya wanafunzi wa China na Afrika yamewawezesha wanafunzi kutoka nchi zinazoendelea kupata elimu ya juu na kutimiza ndoto zao, na wengi kati yao wametafuta ajira mwafaka baada ya kumaliza masomo yao na kuchangia utulivu wa kijamii na maendeleo ya kiuchumi ya nchi zao. Wakati huo huo, mawasiliano hayo yamewapa fursa wanafunzi wa China kuwasiliana na wanafunzi wa kigeni, kuongeza ufahamu wao kuhusu watu na utamaduni wa nchi za kigeni.