Chama cha Waendeshaji watalii Tanzania kinasema madai ya Taasisi ya Oakland hayana msingi
2024-06-18 14:10:40| cri

Chama cha Waendeshaji watalii Tanzania (Tato) kimekemea vikali tuhuma zisizo na msingi zinazotolewa na watendaji wa kigeni wasio wa serikali kuhusu madai ya ukiukwaji wa haki za binadamu nchini Tanzania.

Kauli hii inakuja huku kukiwa na hali ya wasiwasi ndani ya sekta ya utalii ya Tanzania kutokana na ripoti ambazo zimekuwa zikitaka kuchafua sifa ya taifa kwa madai ambayo hayajathibitishwa.

Tuhuma hizo ambazo zinatoka katika Taasisi ya Oakland yenye makao yake makuu California, zinadai kuwa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (Tanapa) limewahamisha wananchi wa eneo hilo kwenye eneo oevu la Usangu ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Ruaha ili kupisha shughuli za utalii.

Bodi ya utalii, yenye waendeshaji wataalamu wa utalii 300 na zaidi, linatetea hatua ya haraka ya serikali ya Tanzania ya kuingiza maeneo muhimu ya vyanzo vya maji ya Uwanda wa Ihefu na Usangu katika Hifadhi ya Taifa ya Ruaha kusini mwa nchi, ikisema uamuzi wa mwaka 2008 ulidhibiti vitendo vingi vya kilimo na ufugaji visivyo endelevu.