Mtoto mwenye ualbino aliyeporwa apatikana ameuawa na kunyofolewa viungo
2024-06-18 14:09:20| cri

Siku 19 tangu mtoto mwenye ualbino, Asimwe Novath (2) anyakuliwe na watu wasiojulikana kutoka mikononi mwa mama yake, mwili wake umepatikana ukiwa umefungwa kwenye kiroba cha sandarusi.

Tukio la Asimwe kupokwa katika mikono ya mama yake lilitokea Mei 30, 2024 katika Kijiji cha Bulamula, Kata ya Kamachumu, Wilaya ya Muleba mkoani Kagera.

Akizungumza Jumatatu Juni 17, 2024, Katibu Tawala wa Wilaya ya Muleba mkoani humo, Benjamin Mwikasyege amethibitisha kupatikana mwili wa mtoto huyo, huku baadhi ya viungo vyake (bila kuvitaja) vikiwa vimenyofolewa.

Mwikasyege amesema mwili wa mtoto huyo umepatikana ukiwa chini ya moja ya karavati iliyoko katika barabara ya Makongora, Kitongoji cha Kabyonda Kijiji cha Balele Kata ya Ruhanga wilayani Muleba mkoani humo.