Vyama vitano vya siasa vyaungana kuunda serikali ya umoja nchini Afrika Kusini
2024-06-18 23:06:26| cri

Chama cha ANC cha nchini Afrika Kusini kimesema jumla ya vyama vitano vya siasa vimesaini taarifa inayoonyesha nia ya kushiriki katika serikali ya umoja wa kitaifa (GNU).

Katika taarifa yake, ANC imesema vyama hivyo ni pamoja na ANC, Democratic Alliance, Inkatha Freedom Party, GOOD na Patriotic Alliance, ambavyo kwa ujumla vinawakilisha viti 273 sawa na asilimia 68 ya wabunge wa nchi hiyo.

ANC imesema, serikali ya umoja wa kitaifa itahakikisha vyama vyote vinavyoshiriki vitakuwa na uwakilishi katika serikali na vyombo vya sheria, kutoa maamuzi kwa pamoja, huku mifumo kwa ajili ya usuluhishi ikipatikana pale inapohitajika.

Katika uchaguzi mkuu uliofanyika Mei 29 mwaka huu, ANC ilipata viti 150 kati ya 400 katika Bunge la Kitaifa, na kwa mara ya kwanza kuwa chini ya asilimia 50 inayotakiwa kudumisha wingi wa wabunge katika bunge la chini uliodumu kwa miaka 30.

Cyril Ramaphosa, kiongozi wa ANC, amechaguliwa tena na Bunge kuwa rais wa nchi hiyo kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.