Zambia yatoa mwito juhudi za pamoja kutatua changamoto za kimataifa zinazokwamisha kutimizwa kwa malengo ya Umoja wa Mataifa
2024-06-18 09:23:59| CRI

Zambia imetoa mwito wa kuimarisha juhudi za pamoja kutatua changamoto zilizopo na zinazoibuka ambazo zinazikabili nchi mbalimbali, ili kutimiza malengo ya maendeleo endelevu ya Umoja wa Mataifa (SDGs).

Katibu wa wizara ya fedha ya nchi hiyo Bw. Felix Nkulukusa amesema, ni muhimu kwa nchi mbalimbali kuimarisha ushirikiano kutatua masuala ya dharura ambayo yameathiri juhudi za maendeleo katika nchi nyingi.

Amesema hayo katika ufunguzi wa mkutano wa mashauriano kuhusu kuandaa ushiriki wa Zambia katika mkutano wa kilele wa siku za baadaye utakaofanyika mwezi wa Septemba, ambao ni shughuli ya ngazi ya juu itakayoshirikisha viongozi wa dunia kufikia makubaliano mapya ya kimataifa kuhusu jinsi ya kujenga siku za leo na kulinda siku za baadaye.