Afisa wa polisi ajaribu kujiua baada ya kupoteza bastola
2024-06-19 23:00:37| cri

Afisa wa polisi aliokolewa Jumatatu akijaribu kujiua nyumbani kwake baada ya kudaiwa kupoteza silaha yake.

Afisa huyo ambaye ni inspekta anayesimamia kituo kimoja cha polisi Kariobangi, Nairobi, na ambaye alikuwa ameripotiwa kutoweka, alisemekana kurejea nyumbani kwake mtaani Ongata Rongai, Jumapili na kumwambia mkewe kwamba amepoteza bastola iliyo na risasi 15 katika hali isiyoeleweka. Kwa mujibu wa ripoti ya polisi, mkewe alisema afisa huyo alionekana kuchanganyikiwa na mwenye mawazo mengi alipokuja nyumbani na hakukumbuka jinsi alivyopoteza bastola hiyo.

“Aliomba radhi na akaenda mahali ambapo huwa tunafua nguo na akameza sumu,” ripoti inamnukuu mkewe akisema.

Alipatikana baadaye akigaragara chini akiwa anakatikiwa na hewa baada ya kudaiwa kumeza sumu hiyo na akakimbizwa hospitalini ambapo amelazwa akiwa anaendelea kupata nafuu.

Polisi baadaye walitembelea nyumba hiyo na kuanzisha msako wa bastola hiyo ambayo bado haijapatikana.