Mapigano yanayoendelea katika mji wa Al-Fashir, jimbo la Darfur Kaskazini nchini Sudan tangu tarehe 10 Mei yamesababisha vifo vya watu wasiopungua 346 na wengine 2,200 kujeruhiwa.
Mkurugenzi mkuu wa wizara ya afya ya jimbo hilo Ibrahim Abdullah Khatir ameliambia Shirika la Habari la Xinhua kuwa idadi hiyo inajumuisha tu vifo na majeruhi vilivyorekodiwa katika hospitali, na idadi halisi ya vifo na majeruhi itakuwa kubwa zaidi.
Kuanzia tarehe 10 Mei, Jeshi la Sudan limekuwa linapambana vikali na Kikosi cha Msaada wa Haraka cha Sudan (RSF) katika mji wa Al-Fashir zikiwania udhibiti wa jimbo la Darfur Kaskazini, ambayo imesababisha vifo na majeruhi kwa raia wengi huku maelfu ya watu wakikimbia makwao.