Kituo cha Kusimamia, Kudhibiti na Kufuatilia Uratibu wa Uvuvi (MCSCC) kilicho chini ya Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) kimeanza kufanya kazi rasmi mjini Maputo, mji mkuu wa Msumbiji, ikiwa ni hatua kubwa katika kupambana na uvuvi haramu na shughuli zisizo halali katika bahari ya kanda hiyo.
Mkutano wa kwanza wa Bodi ya Wakurugenzi wa Kituo hicho umefanyika jana mjini Maputo, na kuzindua rasmi shughuli za kituo hicho.
Waziri wa masuala ya Bahari, Maziwa na Uvuvi wa Msumbiji Lidia Cardoso amesema, kituo hicho kimeundwa ili kuimarisha ushirikiano na uwezo kati ya nchi wanachama wa SADC, na lengo lake kuu ni kumaliza uvuvi haramu katika kanda hiyo.
Amesema mpango wa utendaji wa kituo hicho unajumuisha mikakati ya kukusanya rasilimali na kutekeleza hatua halisi ili kutimiza malengo ya pamoja ya nchi wanachama wa SADC.