Ujumbe wa Mpito wa Umoja wa Afrika nchini Somalia (ATMIS) jana Alhamisi ulimaliza kazi ya kukabidhi kambi nyingine ya kijeshi iliyoko mjini Jowhar, kusini magharibi mwa Somalia, kwa Jeshi la Usalama la Somalia, ikiashiria kuwa ujumbe huo umeanza hatua ya tatu ya kuondoa vikosi vyake nchini humo.
Mhandisi mkuu wa kijeshi wa ATMIS Sleiman Ibrahimi amewahakikishia wasomali kupitia taarifa aliyotoa mjini Mogadishu kuwa hakutakuwa na ombwe la ulinzi wa usalama katika kipindi cha kuondoka kwa vikosi vya ujumbe huo.
Katika hatua mbili za awali za kuondoa vikosi zilizomalizika mwaka jana, ujumbe wa ATMIS uliondoa wanajeshi 5,000 na kukabidhi kambi 17 za kijeshi kwa Jeshi la Somalia. Katika hatua ya tatu, ATMIS imepanga kuondoa wanajeshi 4,000 zaidi nchini Somalia kabla ya mwisho wa mwezi Juni mwaka huu.