Changamoto za watoto wenye hali ya ualbino
2024-06-22 09:00:46| CRI

June 13 ya kila mwaka ni Siku ya Kimataifa ya Uelewa kuhusu Ulemavu wa Ngozi, ama Albino. Lengo kuu la kuadhimisha Siku hii ni kuvuta hisia za watu juu ya tatizo la ubaguzi dhidi ya watu wenye ualbino, ili kuongeza uelewa wa umma ualbino na sababu zake. Mara nyingi kumekuwa na matukio ya watu wenye ulemavu wa ngozi kuuawa kwa imani za kishirikina, wengine wakidiriki hata kuwauza watoto wao wenye ualbino.

Ni kweli matukio hayo yapo, na wanaoathiriwa zaidi ni watoto wanaoishi na hali hiyo. Tumekuwa tukiona na tukisoma kwenye vyombo vya habari kuhusu watoto wadogo wenye hali ya ualbino ama walemavu wa ngozi kuuliwa na baadhi ya viungo vyao kunyofolewa, na wengine kukatwa mikono ilhali wanaona. Lakini kinachoshangaza ni kwamba, inakuwaje mtu mwenye akili timamu, kuamini kuwa kiungo cha binadamu mwenzake kinaweza kumletea utajiri? Ama kwa wanasiasa, kinaweza kumsaidia kushinda katika uchaguzi? Watu wenye ulemavu wa ngozi ni binadamu kama binadamu wengine, na wanapaswa kupata haki zao zote sawa na wengine. Katika kipindi cha leo cha Ukumbi wa Wanawake tutazungumzia kuhusu ualbino na changamoto wanazokutana nazo watu wenye ulemavu huo wa ngozi.